Ijumaa , 24th Mei , 2024

Walimu, wazazi na walezi kata ya Chapwa wilayani Momba wametakiwa kuwa karibu na kuwalinda watoto wao kama mboni za macho ili kujua ukatili wanaofanyiwa katika makuzi kwa lengo la kubaini na kudhibiti mapema kwa kutoa taarifa polisi kwani kufanya hivyo kutapunguza vitendo vya ukatili.

Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Anton Sabasaba Akizungumza wakati alipohudhuria kikao cha wazazi katika Shule ya Msingi Elisabane Mei 24, 2024

Akizungumza wakati alipohudhuria kikao cha wazazi katika Shule ya Msingi Elisabane Mei 24, 2024 Polisi Kata ya Chapwa Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Anton Sabasaba alisema unakuta mzazi hajui mtoto wake ameshindaje, yupo wapi, anacheza na nani na wanacheza michezo gani yeye kutwa na miangaiko yake bila kumuangalia mtoto wake hili linapelekea mtoto kufanyiwa ukatili inapaswa mzazi kufuatilia makuzi ya mtoto wako ili kumuepusha kufanyiwa vitendo vya ukatili na unyanyasajı.

“Mtoto wa mwenzio ni wako pindi umuonapo anacheza michezo ambayo ni hatarishi kwa maisha yake au anafanyiwa ukatili toa taarifa Polisi ili hatua za haraka zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani kwa hatua zaidi alisema Mkaguzi Sabasaba.

Sambamba na hayo Mkaguzi Sabasaba aliwaomba wazazi hao kufikisha elimu hiyo kwa jamii ili watoto wawe salama na waweze kutimiza ndoto za maisha yao ya baadae.

Nae, Marry Aloyce Chaula kwa niaba ya wazazi na walezi katika kikao hicho alimshukuru Mkaguzi Sabasaba kwa elimu aliowapatia na aliahidi kwa niaba ya wazazi waliohudhuria kikao hicho kuendelea kuwafundisha matendo yaliyo mema ikiwa ni pamoja na kuwapa malezi bora watoto wao ili kuwa na kizazi kilicho bora na chenye maadili mema katika ujenzi wa taifa letu.