Jumatatu , 7th Dec , 2015

Idara ya Uvuvi Mkoani Kagera imekamata na kuziteketeza zana za uvuvi haramu zenye thamani ya zaidi ya milioni 641 kutoka kwa wavuvi na wamiliki wa vifaa hivyo mkoani humo.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera John Mongella

Mkuu wa Mkoa wa Kagera John Mongella ambae aliongoza zoezi kuteketeza zana hizo ameipongeza idara hiyo kwa kuendesha operesheni hiyo ambayo imehusisha wauzaji wa Nyavu zilizopigwa marufuku.

Mongela amesema kuwa serikali inabidi kuongeza nguvu zaidi katika kutokomeza uvuvi haramu kwa kuwakamata wahusika zaidi wa uuzaji wa zana hizo haramu za uvuvi ambazo zinatishia kuendelea kwa mazalia ya samaki ziwani.

Idara hiyo imesema imekamata makokoro makubwa 115, pamoja na yale ya dagaa 179, nyavu za macho madogo 647, nyavu ndogo ndogo zaidi ya 1000, vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 641 katika zoezi lililodumu kwa takribani wiki mbili.