Jumatano , 19th Jun , 2019

Msichana Namara George ambaye hakuwahi kumjua mama yake kwa zaidi ya miaka 30, baada ya kutenganishwa naye, amesema moja ya tukio lililomuumiza sana maishani mwake, na kutamani uwepo wa mama yake ili kumfariji.

Akizungumza na www.eatv.tv Namara amesema kwamba, siku ambayo alipata msiba wa kufiwa na mtoto wake, ndipo alipotamani mama yake angelikuwa karibu naye ili amfariji, baada ya kuona kila aliyekuja kumfariji akiondoka nyumbani kwake.

“Unajua baada ya mimi pia kupata mtoto ndio nikajua alichokipitia mama yangu, lakini kama kuna siku niliumia zaidi na kutamani uwepo wa mama, ni pale nilipofiwa na mtoto wangu, kila mtu aliniacha na kuondoka, nikasema mama yangu angekuwepo asingeniacha”, alisikika Namara akisimulia huku akitokwa na machozi.

Namara amesema licha ya baba yake kujitahidi kumlea na kumpa kila alichohitaji, lakini siku zote alikuwa akisali na kumuomba Mungu, amsadie akutane na mama yake, jambo ambalo limetimia kwa mwaka huu baada ya zaidi ya miaka 30 kupita.