Chidi Benz atimiza ahadi yake kwa Juliana Shonza

Ijumaa , 20th Mar , 2020

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza amesema amefurahi kutembelewa na mwana Hip Hop Chidi Benz, ikiwa ni ahadi aliyoitimiza msanii huyo walipokutana katika uzinduzi wa kazi ya Lulu Diva siku ya Machi 13,2020.

Kulia kwenye picha ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza na msanii Chidi Benz

Shonza amesema Chidi Benz alimtembelea ofisini kwake Dodoma, siku ya jana Machi 19 na kumueleza mambo ya msingi kama kujisajili BASATA na kutaka kazi zake zisajiliwe na COSOTA.

Akitoa taarifa hiyo kupitia mtandao wa Instagram ameandika kuwa  "Hiki chuma kipo imara zaidi ya jana, nilifurahi kutembelewa na msanii nguli wa muziki wa BongoFleva Chidi Benz ofisini kwangu Dodoma , ikiwa ni ahadi yake aliyoniahidi nilipokutana naye siku ya uzinduzi wa kazi ya Lulu Diva".

"Kubwa ameniambia anataka kufanya kazi zake za sanaa kiuhalali, kupata usajili wa BASATA pamoja na kusajili kazi zake COSOTA, pia amewashukuru mashabiki, wasanii wenziye na wadau wa muziki kwa kuendelea kumuamini na kumualika kwenye show mbalimbali licha ya changamoto alizopitia" ameongeza.