Jumatatu , 26th Sep , 2016

Baraza la Sanaa Tanzania BASATA limesema Shindano la Dance100% lililomalizika Jumamosi katika viwanja vya Don Bosco Jijini Dar es salaam limewafanya vijana kuwa wamoja na kujenga urafiki.

Mkuu wa Matukio kutoka BASATA Kurwijira N Maregesi

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Matukio kutoka BASATA Kurwijira N Maregesi alipokuwa akitoa tathmini yake kuhusu namna shindano la Dance100% lilivyofanyika mwaka huu kuanzia mwanzo hadi mwisho.

“Dance100% mwaka huu imekuwa na mwamko wa aina yake jambo ambalo linaashiria kwamba jamii inazidi kupata hamasa juu ya shindano na vijana kwa muamko ambao umeonekana wameweza kujenga umoja na mshikamano jambo ambalo ni jema katika jamii” Amesema Maregesi.

Maregesi ameongeza kuwa licha ya mbali umoja ambao umejengeka baina ya makundi ila wengine wanaweza kujipatia ajira kwani shindano hilo limetazamwa na watu wengi na wasanii ambao wanaweza kutaka wachezaji katika kazi zao pamoja na kushiriki shughuli mbalimbali za kitaifa na za kijamii.

Shindano la Dance100% limemalizika kwa kundi la Team Makorokocho kuibuka kidedea na kuondoka na kitita cha milioni 7 wakifuatiwa na kundi la J Combat kutoka Zanzibar ambao wameibuka na kitita cha milioni mbili na kundi lililoshika nafasi ya tatu ni D.D.I Crew ambao wamejipatia shilingi milioni moja.

Matukio yote ya Dance100% 2016 yataoneshwa na EATV siku ya Jumapili saa moja jioni.

Tags: