Jumapili , 1st Sep , 2019

Msanii mkongwe wa Hip Hop na Bongo Fleva nchini na mmiliki wa lebo ya MMB, Madee Ally 'Seneda' amefafanua namna atakavyomtambulisha mke wake kama watu wanavyohitaji kumfahamu.

Madee na mwanaye Chonge

Msanii huyo anayetamba na ngoma yake mpya ya 'Waache waongee' amezungumza kupitia Friday Night Live ya EATV kuwa hayuko tayari kumtambulisha mpenzi au mchumba kwa jamii hivi sasa, bali anahitaji kumtambulisha mke kamili na kusisitiza kuwa atafanya hivyo muda ukifika.

"Wanaotaka niwaoneshe mama Chonge watakuwa wananikosea sana kwa sababu sio tamaduni yangu, mimi nitakuja kuwaonesha mke wangu, "ile pu paa jamani huyu ndiyo mke wangu". Lakini kuwaonesha 'girlfriend' sijui nini, mwisho wa siku tunaweza tusifikie malengo nitataka niwaoneshe tena mwingine", amesema Madee.

Pia Madee amezungumzia kuhusu posti yake nyumba ya hivi karibuni ambayo watu wengi wameichukulia kuwa anajisifu kuwa na nyumba moja wakati yeye ni msanii mkubwa na alipaswa kuwa na nyumba nyingi zaidi ya hiyo.

"Nafikiri watu wahakuielewa vizuri ile posti kwa sababu imeandikwa kisanaa sana, kwa niaba ya watu ambao hawakuelewa ni kwamba ile ni nyumba yangu ya kwanza na ile ni gari yangu ya kwanza. Niko na nyumba kama nne hivi lakini sikuweka posti ile kwa kujisifia hapana".

"Kuna watu wanakata tamaa sana mtaani kwa kuamini kwamba hawajaweza kumiliki vitu vikubwa kwa sababu ya kutokuwa wanamuziki kama mimi, au sio watangazaji wazuri au hawajasoma, kwahiyo tulikuwa tunawkataza kukata tamaa. Kukata tamaa ni dhambi", ameongeza.