Jumatano , 11th Dec , 2019

Mkali wa BongoFleva hapa nchini, Marioo, amesema wasanii wachanga wasitegemee msaada kutoka kwa wasanii wakubwa, kwani mastaa hawana muda kabisa na kwamba hata yeye kabla hajatoka, aliwahi kuipitia hiyo hali ya kutaka kusaidiwa na hakupata msaada wowote.

Msanii wa Muziki nchini, Marioo.

Marioo amefunguka hayo kupitia EATV & EA Radio Digital, wakati akieleza changamoto zake alizokutana nazo kabla ya kuingia kwenye muziki wa BongoFleva.

"Wasanii wengi walinibania ila kitu ambacho nataka niwaambie vijana wenzangu waliopo mtaani na wanataka nafasi, wasitegemee sana 'support' kutoka kwa wasanii kwa sababu wameshasaidia watu wengi ambao wengine wamezingua, hata mimi zamani nilikuwa nakasirika ninapomtumia msanii ujumbe halafu hajibu" ameeleza Marioo.

Marioo ameendelea kusema "Mimi mwenyewe nimeshaumia sana kwenye hayo masuala ya kumpigia msanii simu, halafu anakukatia tena kilichoniumiza zaidi nilimpigia simu mtu ambaye niliamini atanisaidia na ananijua halafu akanipotezea iliniuma sana, ila nimekuja kujua sasa hivi kwamba mastaa wana vitu vingi" ameongeza.