Jumanne , 28th Dec , 2021

Mchezaji wa Simba raia wa Uganda, Thadeo Lwanga, hatima yake ya kuendelea kubakia katika timu ipo mikononi mwa madaktari.

Kiungo huyo mkabaji hivi sasa anajadiliwa na baadhi ya viongozi kwa kile kilichoelezwa kukaa nje ya uwanja kwa msimu mzima kutokana na majeraha ya goti anayoyauguza.

Simba hivi sasa inaelezwa kuwepo katika mazungumzo na kiungo Mbrazili, Gerson Fraga kwa ajili ya kuja kuchukua nafasi yake.

Mmoja wa viongozi aliyetaka jina lake lisitajwe wa timu hiyo, ameliambia kuwa, bado hawajapokea ripoti ya usajili kutoka kwa kocha, Franco Pablo hivyo mara baada ya kuikabidhi itajulikana.

Kiongozi huyo alisema kuwa majeraha ya Lwanga ya kitabibu, wanasubiria ripoti ya daktari kwa ajili ya kuona muda gani atakaa nje ya uwanja.

Aliongeza kuwa kama ripoti hiyo ikieleza kukaa nje kwa muda mrefu, basi watasitisha mkataba wake na kusajili kiungo mwingine mkabaji mwenye kiwango kama chake.

“Kuhusu Lwanga bado Simba hawajafikia maamuzi ya kumuacha ikiwa pia ripoti ya kocha bado hawajaipokea ambayo ndiyo ilitarajiwa kutoka.

“Suala lake lipo kitabibu, hivyo mabosi wanasubiri ripoti ya madaktari wetu wa timu kwa ajili ya kuona muda gani atakosekana,” alisema kiongozi huyo

Alipotafutwa Daktari wa timu hiyo, Yassin Gembe kuzungumzia hilo alisema kwa kifupi: “Mimi sipo na timu, ninaumwa.”