Ijumaa , 18th Aug , 2017

Nahodha wa timu ya Mchenga BBall Stars, Mohammed Yusuph 'Muddy' amefuguka kwa kudai kufungwa ni moja ya njia ya wao kujifunza na kujiweka sawa katika hatua nyingine ya mashindano ambayo yapo mbele yao.

Nahodha wa timu ya Mchenga BBall Stars, Mohammed Yusuph 'Muddy'.

Muddy ameeleza hayo baada ya wao kuchapwa kwa pointi 87-78 na wale waliokuwa wanawadharau na kuwaita vibonde katika michuano ya Sprite BBall Kings ambapo kwa sasa imefikia hatua ya fainali game 2.

"Ukifungwa ni njia moja wapo ya kujifunza katika game inayofuata, kwa kuwa bado tupo katika mashindano na 'best of five'. Tunaenda katika game ya 3 hapo kesho tutaona nani atashinda ila bado tuna nafasi kubwa ya kuwa mabingwa", alisema Muddy.

Pamoja na hayo, Muddy aliendelea kwa kusema "Kilichopelekea mpaka tumefungwa ni kutokana na sisi kucheza kwa kujiachia sana lakini kipigo kipo pale pale", alisisitiza Muddy.

Katika mchezo wa pili Muddy alionekana kukabwa sana na wachezaji wa TMT jambo ambalo lilipelekea Nahodha huyo kushindwa kufurukuta kama anavyokuwaga katika michezo iliyopita katika mashindano haya ya Sprite BBall Kings.