
Mh. Nape Nauye (katikati) akiwa na Katibu Mkuu wa BMT Henry Lihaya (kushoto kwake) na Mwenyekiti wa BMT Deoniz Malinzi (wapili kutoka kulia)
Katika ziara hiyo, imeshuhudiwa Katibu Mkuu wa baraza hilo Henry Lihaya aking’olewa kwenye nafasi hiyo ambapo Mh. Nnauye amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara yake amtafutie nafasi nyingine wizarani.
“Mtendaji mkuu amekaa miaka saba, sasa nadhani inatosha, naagiza katibu mkuu wa wizara ampangie kazi nyingine wizarani kuanzia leo atafanya utaratibu wa kuripoti wizarani kwa katibu mkuu”, amesema Nnauye.
“Halafu kwa mujibu wa sheria ya BMT mwenyekuteuwa mtendaji mkuu ni mwenyekiti wa bodi ambaye nimemwomba alete mapendekezo, sheria inasema atateuwa kwa idhini ya waziri na ndiyo maana nimechukua nafasi ya kuondoka na aliyekuwepo halafu yeye alete mapendekezo mimi nikiridhia atamteuwa ili aje hapa alete chachu mpya”.
“Kwanini tunafanya mabadiliko BMT, ni kwasababu huu ndiyo moyo wa michezo. Tukipabadilisha hapa bila shaka michezo yetu itakwenda vizuri maana hawa ndiyo wanasimamia vyama vya michezo na mtendaji mkuu anakiri kwamba vyama vingi vya michezo havina program za michezo na wenye kusimamia ni hawa”.
“Mtendaji mkuu atakayekuja nitakabananaye koo sana kuhakikisha kwamba anakuwa mkali sana kusimamia program za michezo. Kama hakuna mipango hata usipofanya chochote itaonekana ni sawa tu, lakini ukiwa na mipango unaweza kupima kama utekelezaji unafanyika au haufanyiki kuna maendeleo au hakuna”.
Lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kutekeleza agizo la waziri mkuu la kufanya maboresho kwenye baraza hilo ili liendane na kasi inayotakiwa.
Mh. Nnauye ameahidi kushughulikia changamoto ambazo zinalikabili baraza hilo zikiwemo za fedha, watumishi wachache, matatizo ya sheria na mambo mengine kuhakikisha baraza linaenda sawa.
Baada ya Waziri Nape kumaliza ziara hiyo na kutoa maagizo kwa Mwenyekiti wa BMT Dioniz Malinzi kumteua Katibu Mpya, Malinzi alimteua aliyekuwa Afisa Michezo Mkuu wa TAMISEMI Mohamedi Kiganja kukaimu nafasi ya Katibu Mkuu wa BMT.