Jumatatu , 27th Dec , 2021

Ligi Kuu soka Tanzania bara itaendelea tena leo kwa michezo miwili ya raundi ya 11. Geita Gold FC watakuwa wenyeji wa Mbeya Kwanza na Polisi Tanzania watakipiga dhidi ya Mbeya City.

Mchezo wa mapema unachezwa Saa 8:00 Mchana katika Dimba la Nyankumbu huko Geita, ambapo Geita Gold FC wataminyana na Mabeya kwanza, timu hizi zinatofautiana alama 1 tu kwenye msimamo wa Ligi. Geita ipo nafasi ya 10 ikiwa na alama 11 katika michezo 10 na Mbeya Kwanza ina alama 10 wapo nafasi ya 11.

Wenyeji Geita wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa wametoka kushinda michezo 2 mfululizo iliyopita dhidi ya Tanzania Prisons na Ruvu Shooting na wameshinda michezo 3 kwenye michezo 5 ya mwisho ya Ligi Kuu. Mbeya kwanza hawajawa na muendelezo bora wa matokeo kwani wameshinda mchezo 1 tu kwenye michezo 5 ya mwisho ya Ligi.

Mchezo wa mwisho leo unachezwa Saa 10:00 Jioni kwenye uwanja wa Ushirika Moshi Mkoani Kilimanjaro. Polisi Tanzania wataminyana na timu kizazi Kipya Mbeya City. kwenye michezo 4 ya Ligi kuu waliokutana Polisi hawajaifunga Mbeya City, wamefungwa mara 2 na wametoka sare katika michezo 2. Na msimu uliopita katika Dimba la Ushirika Polisi wakiwa nyummbani walifungwa bao 1-0 na Mbeya City.

Polisi wapo nafasi ya 4 wana alama 16 na wameshinda mchezo 1 tu kwenye michezo 5 ya mwisho, wakati Mbeya City wamefungwa mchezo 1 kwenye michezo 5 ya mwisho wameshinda michezo 2 na sare michezo 2 wapo nafasi ya 6 wana alama 15.