Jumamosi , 8th Aug , 2015

Kumekuwa na kamaida kwa wadau wa michezo mbalimbali hapa nchini kukosoa pale timu au wanamichezo wa mchezo fulani wanapofanya vibaya katika michezo wanayoshiriki hasa ile ya kimataifa sasa wito umetolewa kwao na Serikali kwa ujumla kusaidia michezo

Baadhi ya wanamichezo wa mchezo wa Wushu Kun fu wakionyesha umahiri wao.

Timu ya taifa ya mchezo wa Rollball ambayo inakabiliwa na michuano ya kuwania kombe la dunia itakayofanyika mwishoni mwa mwaka huu nchini India imeendelea na mazoezi ya maandalizi katika viwanja vya chuo kikuu jijini Dar es Salaam.

Mjumbe wa chama cha Rollball Tanzani TRBA na nahodha wa timu hiyo Feruzi Juma ameuambia muhtasari wa michezo kuwa timu hiyo inahitaji kupata mechi za kujipima uwezo ili kubaini mapungufu mapema yafanyiwe kazi na pia kupata angalau uwanja wa kufanyia mazoezi kama ule wa ndani wa taifa.

Aidha Juma ametoa wito kwa wadau na Serikali kwa ujumla kuhakikisha wanatoa sapoti yakutosha kwa michezo midogo kama hii ya RollBall ambao umekuwa na mafanikio katika medani ya kimataifa hasa kwa timu ya Tanzania ambayo imeshapata kushiriki michuano ya dunia mara mbili ikifanya hivyo kwa mara ya kwanza nchini India na baadae kule nchini Kenya.

Kwa sasa kikosi cha timu ya taifa ya Rollball kiko katika maandalizi ya kujiandaa na michuano ya kombe la dunia itakayofanyika nchini India mwishoni mwa mwaka huu hivyo wanahitaji msaada kwa Watanzania ili kufanikisha maandalizi yao hasa kuwawezesha kupata michezo ya kirafiki na timu zilizopiga hatua katika mchezo wa Rollball.

Kwaupande wao chama cha mchezo wa Wushu Kun Fu Tanzania TWA kimewataka wadau wa michezo nchini, makampuni na Serikali kwa ujumla kusapoti michezo midogomidogo hasa ile ya sanaa za kujiami na mapigano ambayo imekuwa ikililetea sifa taifa kwa wanamichezo wake kufanya vema kwa kutwaa medali na mikanda ya ubingwa wa kimataifa.

Na Katibu mkuu wa TWA Sempai Gola Kapipi ameiambia muhtasari wa michezo kuwa ili kuinua sanaa ya michezo ya mapigano wameamua kuandaa shindano maalumu litakalohusisha michezo yote ya mapigano kama kun fu, judo, karate, ngumi na mingine mingi hivyo Serikali na wadau wa michezo wanapaswa kuunga mkono juhudi hizo.

Kapipi amesema kumekuwa na kasumba ya makampuni na hata wadau kuthamini baadhi ya michezo kama soka na kusahau kuwa kuna michezo mingine mingi mikubwa ambayo wao wanaiona kama midogo kwa hapa inaweza kuitangaza nchi kimataifa.