
Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Abdulkarim Amin amesema kocha mkuu wa timu hiyo Aristica Cioaba amependekeza timu hiyo leo iendelee na mazoezi kisha ianze safari kesho kutokana na basi la timu hiyo kuchelewa kutoka Zanzibar.
''Ni kweli tumeahirisha safari hadi kesho, basi la timu lililokuwa Zanzibar limechelewa kufika ambapo limeingia mchana huu, hivyo kocha amependekeza timu iendelee na progaramu ya mazoezi na safari ifanyike kesho'', amesema Abdulkarim.
Jumamosi iliyopita Azam FC ilitwaa ubingwa wa nne wa Kombe la Mapinduzi baada ya kuichapa URA ya Uganda kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90.
Ikiwa Ruvuma Azam FC inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi itacheza na Majimaji siku ya Alhamisi kabla ya kusafiri hadi jijini Mbeya kucheza na Tanzania Prison Januari 22.