Jumatatu , 26th Jul , 2021

Sports Countdown leo Julai 26 2021, stori kali sita (6) ambazo zinatokana na namba 1 mpaka 6 ambapo kila namba inahusiana na stori kwenye Supa Breakfast ya Eastafrica radio kuanzia Saa 1:15 Asubuhi. Na moja ya stori kubwa leo ni pamoja na Simba waichapa Yanga watwaa ubingwa wa FA.

Taddeo Lwanga Mfungaji wa bao pekee la Simba kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Yanga

6. Ni idadi ya mabao ya Ligi kuu England aliyofunga mshambuliaji wa Chelsea Timo Werner msimu uliopita wa 2020-21 akiwa na the blues ambao ulikuwa ni msimu wake wa kwanza baada ya kujiunga na kikosi hicho akitokea Rb Leipzig ya Ujerumani, na kwa mujibu wa ‘Football insider’ imeripotiwa kuwa mshambuliaji huyo anaweza kurejea katika ligi kuu soka nchini Ujerumani Bundesliga katika dirisha hili la usajili la majira ya Joto na anahusishwa kujiunga na mabingwa wa nchi hiyo klabu ya Bayern Munich ambayo kwa sasa inanolewa na kocha Julian Naglesman ambaye alifanya kazi na Werner katika klabu ya Leipzig kwa msimu mmoja wa 2019-20.

Chelsea kwa sasa wanatafuta mshambuliaji wa kati wa daraja la juu ambapo Erling Braut Haaland na Robert Lewandowski wamekuwa wakihusisha kujiunga na matajiri hao wa jiji la London, hii nikutokana na Timo Werner kushindwa kuhishi kwenye matarajio ya Chelsea baada ya kufanga mabao 12 kwenye mashindano yote huku 6 kati ya hayo yakiwa kwenye EPL, msimu wa nyuma wa 2019-20 kabla ya kujiunga na the Blues Timo aliifungia Leipzig mabao 34 na alitoa pasi za usaidizi wa mabao Assist 13 kwenye michuano yote namba ambazo ameshindwa kuwapa Chelsea.

 

5. Ni idadi ya mataji ya Dunia iliyotwaa timu ya taifa ya mpira wa kikapu ya Marekani ambao pia ndio mabingwa watetezi wa mchezo huo kwenye michezo ya Olimpiki na kikosi hicho kimeanza vibaya harakati za kutetea ubingwa wao kwenye Olympic baada ya kufungwa na Timu ya taifa ya Ufaransa kwa alama 83 - 76 kwenye mchezo wa kundi A,

Kipigo hicho ni cha kwanza kwa Marekani kwenye michuano ya Olimpiki baada ya kucheza michezo 25 pasipo kupoteza, na sasa mabingwa hao mara 15 watajiuliza dhidi ya Iran kwenye mchezo unaofata siku ya jumatano.

 

4. Ni miezi ambayo kocha Thomas Tuchel wa Chelsea alitumia kukinoa kikosi cha the Blues na kukiongoza kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa barani ulaya (UEFA champions league) lakini pia kumaliza nafasi ya 4 kwenye ligi kuu Nchini England EPL. Tuchel raia wa Ujerumani alijiunga na Chelsea January 26 akiwa kocha huru baada ya kufutwa kazi na PSG ya Ufaransa na alitwaa mikoba ya kuinoa the blues kutoka kwa Frank Lampard.

Kutokana na mafanikio hayo ambayo aliyapata ndani ya miezi yake 4 tu akiwa na Chelsea Thomas Tuchel ameshinda tuzo ya kocha bora wa mwaka wa Ujerumani tuzo inayotolewa na jarida la michezo la ‘Kicker’ ambapo kura hupigwa na jopo la waandishi wa habari za michezo akipata jumla ya kura 129, akiwashinda makocha kama Hans Flick kocha wa zamani wa Bayern Munich na sasa timu ya taifa ya Ujerumani.

 

3. Ni misimu ambayo mchezaji bora wa Dunia mara 5 Cristiano Ronaldo ameshaitumikia klabu ya Juventus ya Italia ambapo alijiunga na miamba hiyo ya soka ya Italia Julai, 2018 akitokea Real Madrid ya Hispania na sasa mchezaji huyo amebakiza miezi 12 kabla ya kumaliza mkataba wa miaka 4 ambao alisaini wakati anajiunga na kikosi hicho. Makamu wa Rais wa Juventus Pavel Nedved amesema mchezaji huyo atasalia klabu hapo mpaka atakapo maliza mkataba wake mwishoni mwa msimu ujao wa 2021-22.

Kumekuwa na ripoti kuwa Ronaldo ataondoka katika klabu hiyo ya Turin na amekuwa akihusishwa kujiunga na timu zake za zamani Manchester United na Sporting Lisbon lakini pia klabu ya PSG imekuwa ikihusishwa kumuhitaji Ronaldo ambaye wanamtazamia kama mbadala wa Kylian Mbappe anayehusishwa kujiunga na Real Madrid katika dirisha hili la usajili la majira ya Joto.

Ronaldo kwa sasa ana umri wa miaka 36 msimu uliopita alifunga jumla ya Mabao 29 kwenye ligi na alimaliza akiwa kinara wa ufungaji kwenye Ligi Kuu Italia Serie A, na mchezaji huyo anatarajiwa kuripoti mazoezi hii leo tayari kwa maandalizi ya msimu ujao chini ya kocha mpya Massimiliano Allegri .

 

2. Ni ushindi wa Seti mfululizo alizoshinda Naomi Osaka mcheza tennis namba 2 Dunia kwenye mchezo wa raundi ya kwanza kwenye michezo ya Olympic upande wa tennis ambapo amemfunga Zheng Saisai wa China kwa ushindi wa seti mbili kwa 6-1, 6-4, huu ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa Osaka kucheza baada ya miezi miwili tangu alipojitoa kwenye michuano ya wazi ya Ufaransa French open kutokana na tatizo la msongo wa mawazo na alitumia Saa 1 na nusu tu kushinda mchezo huo.

Naomi ndio mchezaji wa daraja la juu aliyesalia baada ya mchezaji namba moja upande wa wanawake Ash Barty kuondolewa kwenye mashindando na Sara Sorribes Tormo kwa kufungwa seti 2 kwa 6-3, 6-4. Na katika round ya pili Naomi Osaka atacheza dhidi ya Viktorija Golubic raia wa Uswiss.

 

1. Ni bao pekee lilofungwa na kiungo mkabaji wa klabu ya Simba SC Taddeo Lwanga kwenye fainali ya kombe la Azam Sports Federation Cup dakika ya 79, na kuipa ushindi timu yake wa bao 1-0 dhidi ya watani zao Yanga SC kwenye mchezo uliochezwa katika dimba la Lake Tanganyika mkoani Kigoma na Simba imefanikiwa kutetea kombe hilo kwa msimu wa pili mfululizo.

Ushindi huu unaifanya timu hiyo ya mabwanyenye kutoka mitaa ya Msimbazi Kariakoo Dar es salaam kuchukua mataji yote mawili makubwa hapa nchini baada ya kuuchukua ubingwa wa Ligi kuu Tanzania bara VPL ambao nao wameutwa kwa msimu wa nne mfululizo, pia katika mchezo huo ilishuhudiwa kiungo wa Yanga Tonombe Mukoko akionyeshwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kiwiko mshambuliaji wa Simba John Bocco, pia huu ni ushindi pekee wa Simba dhidi ya Yanga kwenye michezo 4 waliokutana kwenye mashindano yote ndani ya 2020-21.