Jumapili , 5th Aug , 2018

Msanii wa Hip Hop nchini, Youngkiller ametajwa na nahodha wa Portland Denis Babu, kuwa yeye ndio alikuwa chanzo kikubwa cha ushindi wao dhidi ya Mchenga Bball Stars, kwenye game 2 ya nusu fainali ya michuano ya Sprite Bball Kings, inayoandaliwa na East Africa Television LTD.

Msanii Youngkiller akiwa kwenye mahojiano baada ya mechi ya Portland na Mchenga.

Akiongea baada ya mechi, Denis Babu ambaye aling'aa vyema kwenye mchezo huo, alisema alipomuona msanii huyo ambaye ni rafiki yake mkubwa alipata hamasa ya kuibeba timu ndio maana akafunga pointi 24 kati ya 71 ilizopata timu yake.

''Kwanza Youngkiller hakuniambia kama atakuja uwanjani ila tulipofungwa game 1 nakumbuka aliniambia tutashinda game 2 na game 3 na tutacheza fainali, sasa nilipomuona uwanjani nikakumbuka maneno yake ikabidi nifanye kila njia nisimwangushe ndio maana tumepata matokeo haya'', - alisema.

Youngkiller ambaye ni shabiki wa Portland alijitokeza uwanja wa taifa wa ndani kushuhudia mtanange huo ambapo kama timu yake ya Portland ingefungwa basi ingeaga mashindano lakini yeye mwenyewe alijinasibu kabla ya mchezo kuwa wamekuja kushinda tu na si vinginevyo na ikawa hivyo.

Mchezaji Denis Chibura 'Babu' (mwenye jezi ya kijani) akimiliki mpira kwenye mchezo dhidi ya Mchenga.

Aidha Youngkiller baada ya mechi alipongeza uwepo wa mashindano hayo yanayodhaminiwa na kinywaji cha Sprite na kuweka wazi kuwa rafiki yake huyo (Denis Chibura Babu) amekuwa akimweleza mara kadhaa kuwa lengo lao ni kuchukua ubingwa na zawadi ya shilingi milioni 10 pamoja na zawadi ya mchezaji bora MVP ambayo ni milioni 2. 

Baada ya ushindi wa jana wa pointi 71 kwa 64 Portland na Mchenga sasa zitacheza game 3 Jumatano ya Agosti 8 kwenye uwanja wa Don Bosco kuanzia saa kumi jioni, ili kupata timu itakayocheza fainali na Flying Dribblers ambao jana walitinga fainali kwa kuwafunga Team Kiza pointi 69 kwa 63 ikiwa ni game 2 baada ya game 1 pia kushinda kwa pointi 84 kwa 75.