Ijumaa , 24th Sep , 2021

Mkuu wa Idara ya Habari na mawasiliano wa Azam FC, Zakaria Thabit ametoa wito kwa bodi ya Ligi kuu nchini, (TPLB), kutoa uhuru kwa timu za nyumbani kusimamia maandalizi ya mechi zao, ikiwemo promosheni, bei ya viingilio ili kuweza kuimarisha mapato kwa vilabu.

Mkuu wa Idara ya Habari na mawasiliano wa Azam FC, Zakaria Thabit.

Kauli hii inakuja siku moja baada ya TPLB, kutoa takwimu za mshabiki kwa kila klabu nchini pamoja na vipato walivyovuna kutokana na mauzo ya tiketi za viwanjani kwa msimu wa 2020/2021 huku, Azam wanashikilia nafasi 17 kati ya 18 wakiwa na idadi ya mashabiki 11,456.

Thabit amesema kuwa iwapo vilabu vya ligi kuu vitapewa nafasi na uhuru wa kusimamia maandalizi ya mechi zao, zitaweza kuvuna mapato zaidi ya takwimu zilizotolewa jana, kwakuwa wataelekeza nguvu zaidi kuwashawishi mashabiki kuja uwanjani tofauti na sasa ambapo Bodi ya ligi inasimamia maandalizi hayo nakupanga bei za tiketi ambayo si rafiki kwa  maendeleo ya vilabu.

Msemaji wa wanalamba lamba hao wa chamanzi, ameomba Bodi ya ligi kuu kurejea upya ratiba ya Azam, hususani kwenye michezo yao ya nyumbani ambazo nyingi huchezwa majira ya usiku na katikati ya juma zikawia ugumu watazamaji kujitokeza kutokana na majukumu yao binfasi.