
Real Madrid imeshinda michezo 2 ya La liga mfululizo kwa mara ya kwanza mwaka 2021
Mabao ya Madrid usiku wa jana yalifungwa na Karim Benzema dakika ya 60 na hilo ni bao lake la 16 msimu huu kwenye mashindano yote na la 11 kwenye la liga, bao la pili limefungwa na Mlinzi Ferland Mendy aliyefunga dakika ya 66.
Kwa ushindi huo Madrid imepanda mpaka nafasi ya pili ikifikisha alama 46 ikiwa ni alama 3 juu ya mahasimu wao FC Barcelona walio nafasi ya 3 na tofauti ya alama 5 na vinara Atletico Madrid wenye alama 51, lakini wakiwa wamecheza michezo 2 pungufu.
Baada ya mchezo huo Zidane alisisitiza kuwa mpango wao ni kuhakikisha wanashinda kila mchezo wakiwa na lengo la kutetea ubingwa.
"Haitabadilisha chochote, tutafanya kazi yetu. Wajibu wetu ni kupigana, kuendelea na kazi yetu, bila kuwajali wengine. Ni ushindi mzuri, ushindi wa pili mfululizo na tulihitaji pia tunamajeruhi wengi. Sidhani kuna mashabiki wa Madrid ambao wanadhani tutapoteza ubingwa. Kinyume chake, wanafikiri tunaweza kubadilisha vitu kila wakati na hicho ndicho tunajaribu kufanya”, alisema Zidane.
Ushindi wa usiku wa jana ni wa pili mfululizo kwa Los Blancos ambao ndio mabaingwa watetezi wa La liga, baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Huesca siku ya Jumamosi, ikiwa ni kwa mara ya kwanza kikosi hicho kinashinda michezo 2 mfululizo ndani ya mwaka 2021.