Ijumaa , 23rd Nov , 2018

Klabu ya soka ya Lipuli FC imekuwa timu ya kwanza katika msimu miwili mfululizo kugoma kufungwa na Simba katika uwanja wa taifa baada ya leo kutoka suluhu kwenye mchezo wa ligi kuu soka Tanzania bara.

Wachezaji wa Lipuli FC na Simba kwenye mchezo wa leo.

Lipuli FC sasa wamejiwekea rekodi ye pekee ikiwa ndio timu iliyopanda ligi kuu na kushindwa kuruhusu kufungwa na Simba ndani ya michezo mitatu waliyokutana.

Novemba 26, 2017 ikiwa kwenye msimu wake wa kwanza Lipuli ilitoka sare ya 1-1 kwenye uwanja wa taifa ambapo ilikuwa ni mechi ya ligi kuu raundi ya kwanza. Bao la Simba lilifungwa na Mwinyi Kazimoto huku la Lipuli FC likifungwa na Asante kwasi ambaye kwasasa ni mchezaji wa Simba.

April 21, 2018 Lipuli wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Samora mjini Iringa walitoka sare ya bao 1-1 na Simba hivyo kukamilisha msimuwa 2017/18 bila kufungwa na Simba ambao waliibuka mabingwa. Bao la Lipuli lilifungwa na Adam Salamba huku lile Simba likifungwa na Laudit Mavugo.

Kwa matokeo hayo Simba wanaendelea kubaki katika nafasi ya 3 wakiwa na alama 27 kwenye mechi 12, huku Lipuli FC wakitoka nafasi ya 17 hadi 14 wakiwa na alama 13.

Azam FC wao wanabaki kileleni wakiwa na alama 33 kwenye mechi 13 wakifuatiwa na Yanga yenye alama 29 kwenye mechi 11.