Jumatano , 15th Dec , 2021

Mshambuliaji wa klabu ya FC Barcelona Sergio Kun Aguero ametangaza kustaafu rasmi kucheza soka la kulipwa kutokana na matatizo ya ugonjwa wa moyo, mshambuliaji huyo ameitumikia klabu hiyo kutoka Catalunya katika michezo mitano pekee tangu ajiunge nayo akitokea Manchester City.

Sergio Kun Aguero

Agüero mwenye umri wa 33 amefikia hatua hiyo ya kustaafu baada ya tatizo la Moyo kuonekana kuwa kubwa kuliko ilivyodhaniwa hapo awali, mshambuliaji huyo wa zamani wa Atletico Madrid na Manchester City alipata shida ya Moyo kwenye mchezo wa Ligi Kuu nchini Hispania La Liga dhidi ya Alaves uliochezwa Oktoba 31, 2021 ambapo alipata shida ya kupumua na baadae ikagundulika kuwa anatatizo la moyo la (heart arrhythmias) ambalo husababisha mapigo ya Moyo kudunda zaidi ya kawaida.

Ripoti za awali za Madaktari zilionyesha Aguero alipaswa kupumzika kwa muda wa miezi mitatu, lakini baada ya tatizo kuonekana kuwa kubwa akashauriwa astaafu kucheza soka, na leo kwenye hafla fupi ya kumuaga Aguero amesema “afya ndio kipaumbele cha kwanza kwangu, madaktari wamenishauri ni vyema nikaacha kucheza soka kwa hiyo natangaza kustaafu soka na kuondoka ndani ya FC Barcelona”.

Raia huyo wa Argentina amecheza michezo 786 na kufunga magoli 427 kwa ngazi ya klabu na timu ya taifa ya Argentina huku akijivunia kubeba mataji makubwa zaidi ya 20 kwenye maisha yake ya soka, ikiwemo mataji matano ya Ligi Kuu England akiwa na Manchester City.