Jumapili , 12th Oct , 2025

Hatua hiyo inatokea zikiwa zimesalia siku 17 tu kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29,2025.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imefanya marekebisho katika maeneo ya uchaguzi ikiwemo kuzifuta kata 10, kutengua na kuwaondoa wagombea udiwani saba.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo Jumapili Oktoba 12, 2025 na kusainiwa na Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele, uamuzi huo umefikiwa baada ya tangazo la Serikali Na. 596 namba 600 la Oktoba 3, 2025, ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) alitangaza marekebisho ya mipaka ya maeneo ya utawala na kufuta kata kadhaa.

Kwa mujibu wa INEC, kata zilizofutwa ni Litapunga, Kanoge, Katumba, Mishamo, Ilangu, Bulamata, Ipwaga, Milambo, Igombemkulu na Kanindo. Aidha, tume imetengua uteuzi na kuwaondoa katika orodha ya wagombea udiwani saba walioteuliwa katika kata husika ambao wote kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), akiwemo Salehe Mrisho Msompola (Kata; Kanoge), Elius Wilson Elia (Kata: Katumba).

Wengine ni Mohamed Ally Asenga (Kata: Litapunga), Nicas Athanas Nibengo (Bulamata), Sadick Augostino Mathew (Ilangu), Rehani Simba Sokota (Ipwaga) na Juma Mohamed Kansimba (Mishamo).
Taarifa hiyo imeeleza kuwa INEC imelazimika kufuta vituo 292 vya kupigia kura vilivyokuwa kwenye kata zilizofutwa.

Hatua hiyo inatokea zikiwa zimesalia siku 17 tu kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29,2025.