Thursday , 16th May , 2019

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameeleza amepokea taarifa ya kufanyiwa ukaguzi kwa ofisi ya CAG Profesa Assad, ambao umefanya na kampuni binafsi na yeye kuikabidhi kwenye kamati ya PAC na kueleza baada ya uchambuzi ataisoma taarifa hiyo bungeni.

Spika Ndugai ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma wakati wa muendelezo wa vikao vya Bunge la 11 jijini humo, ambapo amedai kuwa katika suala la ukaguzi hakuna taasisi inayolikwepa.

Spika Ndugai amesema kuwa, "ningependa kuwajulisha juu ya taarifa ya  ukaguzi wa ofisi ya CAG kwa mwaka fedha unaoshia Juni, 2018, hesabu za CAG zinapaswa kukaguliwa walau mara moja kwa mwaka, na Kamati ya PAC ndiyo inajukumu la kukagua ofisi hiyo, kazi imeshafanyika na imetuletea taarifa ya hesabu zilizokaguliwa za ofisi hiyo."

Aidha Spika Ndugai amesema kuwa, "taarifa ya kukaguliwa ofisi ya CAG, nimeshaipitia kuna mambo, lakini kiutaratibu nimeshaipeleka PAC na wakishamaliza uchambuzi watawasilisha kwangu, niwataarifu kwenye masuala ya ukaguzi hakuna anayebaki kila watu wanawakagua wenzao."

Spika Ndugai na CAG Assad wamekuwa kwenye mgogoro wa muda mrefu kufuatia mara ya kwanza CAG akiwa nje ya nchi kutoa kauli ambayo ilionesha kulidhalilisha Bunge la Tanzania kwa kudai kuwa Bunge hilo ni dhaifu.