Thursday , 21st Dec , 2017

Jeshi la Polisi Mkaoni Mwanza kwa kushirikiana na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamethibitisha kushikiliwa mfanyabiashara Emmanuel Munisi mkazi wa Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza akiendesha kiwanda,

cha kuzalisha pombe bandia aina ya Shujaa kinyume cha sheria.

Mfanyabiashara huyo anadaiwa kujenga kiwanda na kuzalisha pombe kali aina ya  Shujaa 'Portable Spirit' pombe ambayo ni hatari kwa usalama wa watumiaji kutokana na kutothibitishwa ubora wake na mamlaka inayohusika ikiwa ni pamoja na kutolipa kodi stahiki.

Meneja wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Ziwa Moses Mbambe  amesema pombe inayotengenezwa na kiwanda hicho ni hatari kwa maisha ya wanywaji.

Naye Meneja Msaidizi wa upande wa madeni na ushurutishaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mwanza, Beatus Maro ametilia shaka uhalali wa Stampu za TRA zilizokutwa katika kiwanda hicho.

"Katika kudhibiti utengenezaji  holela wa hivi viti, tunatoa hizi 'stamp' mbali na kibali. Naona hizi 'Stamp' hapa, kwa sasa sijui ni sahihi au sahihi kwani inahitaji utaalam kubaini. Lakini  kama inavyoonekana kiwanda hichi hatujakipa kibali hivyo si rahisi awe na hizi 'stamp," amesema Beatus

Hata hivyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Ahmed Msangi amesema jeshi hilo linawashikilia watu wanne akiwemo mmliki wa kiwanda hicho na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara uchunguzi utakapokamilika.