Wednesday , 5th Oct , 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuchunguza sababu za Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma Bw Antonino Kilumbi kutengeneza madawati kwa watu binafsi badala ya karakana ya Magereza kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea Gereza la Isanga mkoani Dodoma

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo wakati alipotembelea Gereza la Isanga mkoani Dodoma akiwa kwenye ziara ya kukagua maeneo yanayotoa huduma za jamii ambapo amesema kuwa Magereza mkoa wa Dodoma ilipewa sh. milioni 24 na Serikali ili kutengeneza madawati 480 na kila moja lilitakiwa kugharimu sh. 50,000.

Uongozi wa gereza hilo uliwapa watu binafsi kutengeneza madawati hayo na kugharimu sh. 70,000 kwa dawati moja ambapo waziri amehoji kama gereza hilo halikuwa na uwezo wa kutengeneza madawati hayo kwa nini kazi hiyo wasingeipeleka kwenye taasisi nyingine ya umma, hivyo kumtaka Mkuu wa Mkoa Bw. Rugimbana kufuatilia ziada ya sh. 20,000 kwenye utengenezaji wa kila dawati.

“Nimesikia kwamba mnawachangisha askari kiasi kilichoongezeka kwenye utengenezaji wa madawati hayo. Ni marufuku askari kutoa fedha mifukoni mwao kulipia shughuli za Serikali,” amesisitiza.

Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma Bw. Kilumbi amesema waliamua kupeleka kazi hiyo kwa watu binafsi kwa sababu hawana vifaa.

Aidha, Waziri Mkuu amemtaka mkuu huyo wa magereza mkoa kuimarisha kitengo cha ufundi seremala na kuhakikisha anatumia vizuri nguvu kazi aliyonayo katika kuzalisha bidhaa mbalimbali.