Thursday , 21st Dec , 2017

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Kamishna Msaidizi Muandamizi wa Polisi (SACP), Wilbroad Mutafungwa amesema ni  kweli jeshi la Polisi Mkoani kwake linashikilia fuvu linalosadikiwa kuwa ni la kichwa cha binadamu kwa ajili ya uchunguzi.

Kamanda Mutafugwa  amesema jeshi lake  linafanya uchunguzi wa fuvu  hilo linalosadikiwa kuwa ni la binadamu lililokutwa katika mgodi mdogo wa dhahabu wa kitunda wilayani Sikonge Mkoani Tabora , ili kubaini kuwa ni la nani na alifariki katika mazingira gani.

"Ni kweli jeshi la Polisi Mkoani Tabora linafanya uchunguzi kuhusiana na tukio la kuonekana kwa fuvu linalosadikiwa kuwa ni la binadamu tukio lenyewe lilitokea huko wilayani Skonge katika mgodi wa wachimbaji wadogo wadogo wa Kitunda katika shimo ambalo hapo awali walikuwa wanachimba kampuni ya Kipumba mines”, amesema.

Kamanda ameongeza kuwa wachimbaji wa mgodi huo waliona fuvu la kichwa hicho kinachosadikiwa kuwa ni cha binadamu na hatimaye kutoa taarifa kwa askari  ambao hufanya doria maeneo hayo.

“Askari wetu walifika hapo na kuchukua fuvu hilo linalosadikiwa kuwa ni kichwa cha binadamu na kulihifadhi kwa ajili ya uchunguzi, ni fuvu tu bila kiwiliwili kwahiyo sasa tunafanya uchunguzi tukishirikiana na hospitali", amesema Kamanda Mutafungwa.

Kamanda Mutafugwa amewaomba wananchi wawe wavumilivu katika kipindi hiki  ambacho jeshi la Polisi linafanya uchunguzi, na  uchunguzi utakapokamilika watatoa taarifa zaidi ya tukio hilo.