Wednesday , 5th Oct , 2016

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako anakusudia kupeleka Muswada Bungeni wa kuunda chombo cha kitaaluma ambacho kitawasimamia waalimu na kuwapa usajili kwa mujibu wa sheria kabla ya kupewa ajira.

Prof. Joyce Ndalichako

Prof. Joyce Ndalichako amesema, Muswada huo ni miongoni mwa mikakati ya kuinua ubora wa elimu na kuleta matokeo chanya ambayo yatawawezesha kupata wahitimu wenye kusheheni maarifa na ujuzi kulingana na elimu waliohitimu.

Ameongeza kuwa Muswada huo pia utatoa mwongozo wa namna vyuo vikuu vyote hapa nchini vitajiendesha sambamba na viwango vya ubora vitakavyohitajika kuwa navyo.

"Muswada huo tumeuandaa na tayari umeanza kujadiliwa katika ngazi mbalimbali kulingana na hatua zilizopo ili kufikia mwakani mwezi wa pili tutauwasilisha Bungeni kwaajili ya kupitishwa na kuwa sheria ili tuweze kuwa na waalimu wenye sifa kulingana na vigezo vitakavyowekwa" amesema

Prof. Ndalichako amekiri ubora wa elimu umeshuka licha ya hatua kadhaa kuchukuliwa na kushindwa kufanikiwa, hivyo hayuko tayari kumbeba mtu yeyote asiye na sifa na kuwataka wananchi kutolaumu hatua zinapochukuliwa na serikali kwani zinalenga kuleta ubora wa elimu.

Wastaafu wa sekta ya elimu wamekaa na waziri huyo kwalengo la kujadili namna ya koboresha elimu ambapo Prof. Henry Joseph Mosha ambaye ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Dar es salaam na Oliver Mhaiki ambaye ni mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Waalimu amesema serikali ihakikishe mtoto anajua kusoma, kuandika na kuhesabu kabla ya kufika darasa la nne.