Wednesday , 5th Oct , 2016

Mamlaka ya Mapato nchini Tanzania (TRA) imeanza zoezi la ukaguzi wa mizigo inayosafirishwa kwa njia ya magari maeneo yote nchini.

Richard Kayombo

Katika ukaguzi huo, kwa kushirikiana na maafisa wa idara nyingine za serikali, TRA itakuwa ikikagua kuhakiki iwapo mizigo iliyobebwa imelipiwa risiti za kielektroniki huku wamiliki wa mizigo nao wakitakiwa kuonyesha risiti ya gharama za usafirishaji wa mzigo husika

Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipakodi wa TRA Bw. Richard Kayombo, amesema hayo leo na kwamba hatua hiyo inalenga kudhibiti upotevu wa mapato unaofanywa kupitia mizigo inayosafirishwa kwenye malori sambamba na kuhakikisha wasafirishaji wa malori wanalipa kodi na ushuru kama zilivyo biashara nyingine.

Aidha, Kayombo amezungumzia zoezi la ukusanyaji wa mapato ambapo kwa mwezi Septemba pekee, mamlaka hiyo imefanikiwa kukusanya shilingi trilioni 1.37 na kufanya jumla ya makusanyo katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo wa mwaka huu wa fedha kufikia fedha za Tanzania shilingi trilioni 3.59.