Tuesday , 1st Mar , 2016

Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Momba mkoani Songwe kimewataka madiwani wa halmashauri ya wilaya kujenga umoja na mshikamano pasipo kubaguana kutokana na itikadi za vyama.

Kikao cha balaza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Momba

Mwenyekiti wa CCM wilayani humo Eliakim Simpasa ametoa nasaha hizo kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Momba kilichokuwa maalumu kwajili ya kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017.

Simpasa amesema kuingizwa kwa itikadi za vyama katika utoaji maamuzi ya halmashauri kunaweza kusababisha mambo ya msingi kukwama na hivyo kusababisha wanancho kutonufaika na vipaumbele wanavyoviibua kwenye maeneo yao.

Amewataka madiwani hao kuwa mfano wa kuigwa na halmashauri nyingine kwa kufanya kazi kwa umoja kwakuwa nyumba wanayojenga ni moja hivyo hakuna haja ya kugombania fito.

Simpasa pia amesema ushirikiano baina ya madiwani na wataalamu wa halmashauri ni jambo muhimu kwakuwa pande hizo mbili zinategemeana katika utekelezaji wa majukumu wenye tija kwa jamii zinazoitumikia.

Amesema tabia ya madiwani kujenga ukuta kati yao na watendaji ndiyo chanzo cha kuzorota kwa maendeleo ya halmashauri kwakuwa wakati madiwani wakipanga kuwaazimia watendaji, wao watakuwa wakipanga kukwamisha mikakati inayowekwa na vikao vya baraza.