
Rais wa Chama cha walimu nchini, Gratian Mukoba
Mukoba ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika kipindi cha East Africa Breakfast ikiwa leo ni siku ya walimu duniani ambapo ameshiriki katika kipindi kuzungumzia sekta ya elimu nchini na maslahi ya walimu kwa ujumla.
“Wanafunzi kwa sasa hivi hawafundishwi kuelewa mambo yanayoendelea na yanayohusu mazingira yao, wanafundishwa kujibu mitihani ndiyo maana walimu wanatumia mitihani ya miaka minne iliyopita kuwafundisha wanafunzi ili wajibu mitihani kwa namna hiyo na siyo kuelewa uhalisia wa mambo, jambo ambalo linazalisha vyeti vya ufaulu wa wanafunzi ambao hawajui kitu” Amesema Mukoba.
Aidha Mukoba amezungumzia suala la malimbikizo ya walimu na kusema kuwa walimu ni kweli wanaidai serikali ila katika mahesabu ambayo huyapeleka watendaji wa Halmashauri huongeza fedha hizo ndiyo maana kunakuwepo na malipo hewa kunapofanyika ukaguzi.
Pamoja na hayo Muboba amesema kuna baadhi ya walimu ambao wameonewa kutokana na zoezi la wanafunzi hewa kwa kuwa idadi ambazo zimetolewa na viongozi siyo ambazo zilitolewa na wakuu wa shule.
Kuhusu nyumba za walimu Mukoba ameiomba serikali kutazama upya idadi ya wanafunzi na uwiano wa walimu ambao wapo katika shule, kwani wanafunzi ni wengi huku nyumba za walimu waliopo zikiwa hazitoshi, jambo ambalo linaondoa morali ya walimu katika kazi.