Thursday , 21st Dec , 2017

Baada ya Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu ya Simba Zacharia Hans Poppe kusema wametuma barua ya kutaka kumsajili beki wa Lipuli FC Asante Kwasi, timu hiyo kutoka Iringa imejibu kwa kuwakaribisha mezani.

“Tayari tumepokea barua ya Simba, wamesema wanamhitaji Kwasi na sisi hatuna shida, tunawakaribisha mezani kwaajili ya mazungumzo na kama tutakubaliana basi suala hilo litamalizika, ” amesema msemaji wa klabu hiyo Clement Sanga.

Mapema leo Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya vinara wa ligi msimu huu Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema wamepeleka barua kwa Lipuli FC baada ya kugundua bado ana mkataba na klabu hiyo.

Kumekuwa na sintofahamu kuhusu usajili wa mlinzi huyo wa kati raia wa Ghana ambaye anafanya vizuri ndani ya klabu ya Lipuli FC akiwa amefanikiwa kufunga mabao matano hadi sasa. Simba inalazimika kumsajili Kwasi baada ya kuachana na beki wake Method Mwanjali raia wa Zimbambwe.