Tuesday , 14th Mar , 2017

Msemaji wa klabu ya Simba Haji Manara amesisitiza kuwa beki wa klabu hiyo Method Mwanjali hatakuwemo kwenye kikosi kitakachoshuka dimbani siku ya Jumapili kupambana na Madini FC ya Arusha, kutokana na kuwa majeruhi.

Haji Manara - Msemaji wa Simba

Manara amesema kuwa taarifa kuwa beki huyo atacheza katika mchezo huo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho siyo za ukweli kwa kuwa taarifa ya madaktari inaonesha kuwa Mwanjali bado hajaimarika kiafya.

“Method bado anaendelea na matibabu na ni lazima tuwe wakweli hatatumika kwenye mechi dhidi ya Madini, tunatarajia labda anaweza kuanza kutumika kwenye mechi za Kanda ya Ziwa kama kocha ataona tayari lakini madaktari wametuhakikishia baada ya mechi dhidi ya Madini ataanza mazoezi mepesi”. Alisema Manara

Vilevile msemaji huyo aliendelea kufunguka kwa kuweka bayana kuwa siyo Method peke yake ambaye atakuwa nje ya uwanja ila mpaka Jamal Mnyate kutokana na majeruhi ya muda mrefu.

Method Mwanjali siku alipoumia

Mwanjali amekuwa nje ya uwanja tangu Februari 11, 2017 alipoumia goti wakati Simba ikicheza dhidi ya Tanzania Prisons kwenye uwanja wa Taifa na kupata ushindi wa magoli 3-0 na hadi sasa amekwisha kosa mechi mbili za ligi kuu Tanzania bara ikiwemo dhidi ya Yanga ambayo Simba iliondoka na ushindi wa mabao 2-1