
Kikosi cha Serengeti Boys
Timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Tanzania (Serengeti Boys), imefuzu hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi ya fainali za Afrika mwakani nchini Madagascar, baada ya kuifunga Afrika Kusini mabao 2-0 jioni ya leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Huku ikicheza pungufu tangu dakika ya 44, baada ya kiungo wake wa ulinzi, Ally Hamisi Ng’anzi kuoneshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu, ahsante nyingi kwao, wafungaji wa mabao hayo leo, Mohamed Rashid Abdallah kipindi cha kwanza na Muhsin Malima Makame kipindi cha pili.
Serengeti Boys, sasa itamenyana na mshindi wa jumla kati ya Kongo Brazaville na Namibia katika hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi ya Madagascar mwakani.