Wednesday , 5th Oct , 2016

Mwamuzi Ahmed Seif amefungiwa miezi sita kwa kushindwa kumudu mechi kati ya African Lyon na Mbao FC ikiwemo kutoa adhabu ya penalti ambayo haikuwa sahihi.

Boniphace Wambura, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi

Pia Mwamuzi huyo alipata alama za chini ambazo hazimruhusu kuendelea kuchezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom.

Katika mchezo huo uliopigwa Septemba 12 katika uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, African Lyon ilipata ushindi wa mabao 3-1.

Afisa Habari wa TFF Bwana Alfred Lucas amesema kuwa adhabu hiyo ni baada ya kikao cha Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi kilichakaa jana, ambacho kimepitia michezo mbalimbali ya ligi kuu na ligi daraja la kwanza, na kutoa adhabu kwa vilabu vingine mbalimbali ambapo maamuzi mengine yako kama ifuatavyo.

JKT Ruvu imepewa onyo na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya Msimamizi wa Kituo, na Ofisa wa Bodi ya Ligi kushambuliwa na mshabiki wa timu hiyo katika mechi dhidi ya Mbeya City iliyofanyika Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

Mshabiki huyo amefungiwa miezi 12, na iwapo vitendo hicho vitaendelea Uwanja huo utafungiwa kwa mechi za Ligi Kuu.

Klabu ya Azam FC imepigwa faini ya sh. 3,000,000 (milioni tatu) kwa kuvaa nembo ya mdhamini wa Ligi Kuu kwenye mkono mmoja badala ya miwili katika mechi yao dhidi ya Ruvu Shooting.

Taarifa iliyotolewa leo na Afisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, imesema kuwa kitendo hicho ni kinyume na Kanuni ya 13(1), na na kwamba adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 13(6) ya kanuni za uendeshaji wa ligi.

Pia Makamishna David Lugenge na Godbless Kimaro wamepewa onyo kwa kuwasilisha taarifa zenye upungufu katika mechi walizosimamia za raundi ya tano na saba.

Katika Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Mbeya Warriors imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kupitia mlango usio sahihi ikiwemo kuvunja kufuli kwenye mechi kati yao na Kimondo FC iliyofanyika Septemba 24 mwaka huu Uwanja Vwawa mkoani Songwe. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(48) ya Ligi Daraja la Kwanza.