Thursday , 21st Dec , 2017

Wavuvi zaidi ya 300 na wauzaji samaki katika eneo la Malindi nchini Kenya, wamesitisha biashara zao kulalamikia kunyanyaswa kwa wavuvi wa kigeni wanaotoka kisiwani Pemba nchini Tanzania ambao wanafanya shughuli zao eneo hilo 

Tukio hilo limetokea baada ya polisi kukamata wavuvi 10 wanaosemekana wametoka Tanzania kwa madai kwamba wamo humu nchini kiharamu.

Bw. Simon Kitsao, mvuvi ambaye anafanya kazi pamoja na wenzake wa Tanzania amesema kukamatwa kwa wenzao mara kwa mara huathiri biashara ya uvuvi na huenda wauzaji wa samaki wakabaki bila kazi.

“Wavuvi wa humu nchini hawana uwezo wa kuvua kiwango cha kutosha cha samaki kinachohitajika sokoni. Hawa wenzetu ni wataalamu na huvua samaki wengi sana. Huwa tunaungana nao ili tujifunze mbinu zao, Watanzania ni ndugu zetu na tumeishi kwa umoja tukafanya biashara pamoja kwa muda mrefu kwa kiwango cha kuwa wengine wao wameoa eneo hili,” alisikika akisema mvuvi huyo.

Mwenyekiti wa Kitengo cha Usimamizi wa Ufuo wa Mayungu, Bw Ahmed Omar akitetea suala hilo amesema kitengo hicho ndicho hualika Watanzania nchini Kenya kwa sababu kuna hitaji kubwa la samaki.

“Hatua hii imeleta nafasi za ajira kwa karibu vijana na wanawake 500 na hivyo basi kupunguza uhalifu katika eneo hili,” akasema.