
Kamanda wa Jeshi la Uhamaji mkoani Arusha, Mrakibu Mwandamizi Samweli Mahirane
Mkoa wa Arusha ni maeneo ambayo yamekuwa na changamoto ya wahamiaji haramu ambao hutumia njia za panya kuingia nchini hii ikiwa ni kutokana na mkoa huo kupakana na baadhi ya nchi za Afrika Mashariki ikiwemo nchi ya Kenya, hali ambayo inalilazimu jeshi la uhamiaji kuwa makini zaidi kudhibiti uhalifu zaidi
Haya yanabainishwa jijini Arusha na Kamanda wa Jeshi la Uhamaji mkoani Arusha, Mrakibu Mwandamizi Samweli Mahirane wakati akizungumza na vyombo vya habari ambapo ameongeza kuwa jeshi hilo halitamvumilia askari au mtendaji yoyote atakaye jihusisha na vitendo vya rushwa katika utekelezaji wa majukumu ya jeshi.
Samwel Mahirane amesema, "tunafanya kazi mchana na usiku na kazi zetu sisi ni za muda wote, tunaweka vizuizi na kama unavyoona kwa mtiririko huu hata sasa ile trend ya wahamiaji haramu waliyokuwa wakiifanya Arusha kuwa njia, namba yao imepungua na hiyo ni kwa sababu ya ukali tulionao dhidi ya hao watu na kazi tunazozifanya masaa 24".
"Mtu akikuomba pesa sasahivi kimbia moja kwa moja, nenda TAKUKURU, Jeshi la Polisi au ukiogopa sana basi muone hata Mkuu wa Mkoa kwa sababu tuna ushirikiano mwema na anatuongoza vyema kwa shughuli zetu za kiutendaji. Kamwambie kuna mtu amenifanyia hivi na mimi ataniambia na nitachukua hatua haraka sana", ameongeza.