
Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji, John Masunga
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo alipofanya ziara ya kikazi katika Makao Makuu ya Jeshi hilo, jijini Dodoma, ambapo amesema licha kuwepo kwa upungufu wa vifaa bado wanatakiwa wawahi kwenye matukio.
"Jambo lingine ambalo tumelisisitizia, tumeelekeza na tumeamuru wafanye hivyo wawe wanawahi mapema kwenye matukio , matukio mengi yanatokea mpaka kama ni majengo au sehemu nyingine yeyote inateketea na wao hawajafika mwisho wa siku wananchi wanapoteza imani na jeshi hili" amesema Chilo
Akizungumzia juu ya hoja ya kuchelewa kufika katika matukio Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji, John Masunga amesema sababu ya kuchelewa kufika kaatika matukio ni kuchelewa kwa taarifa kutoka kwa wananchi ambao huanza kushughulikia tatizo wenyewe.
"Tukio likitokea wananchi wanaanza kuhangaika wenyewe kuzima moto wakiona unawashinda basi wanapiga simu kwa jeshi la zimamoto tunapofika pale moto unakuwa umeshasababisha madhara makubwa, sababu ya pili maeneo mengi si rafiki kiasi kwamba inakuwa vigumu kwa magari yetu ya zimamoto kufika kwenye maeneo yale, lakini pamoja na changamoto hizo tunaahidi tutajitahidi zaidi na zaidi kuhakikisha tunafika kwenye matukio haraka iwezekananvyo" amesema Kamishna Jenerali wa Zimamoto na Uokoaji John Masunga