Monday , 7th Jun , 2021

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Mhe. David Silinde, amesema michango inayoruhusiwa katika suala la elimu ni uchangiaji wa hiari na hauhusishi wanafunzi kuzuiwa kuhudhuria masomo.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, Mhe. David Silinde

Mhe. Silinde amesema hayo katika kipindi cha maswali na majibu, leo bungeni, akijibu swali lililoulizwa na mbunge wa Nkasi Kaskazini Mhe. Aida Khenani lililotaka kujua kwanini serikali inasema elimu ya shule ya msingi na sekondari ni bure wakati wazazi wanaendelea kuchangishwa michango ya elimu.

“Waraka wa elimu namba 5 ulishazungumza elimu msingi ni elimu bila ada, waraka wa elimu namba 3 wa mwaka 2016, unaeleza wajibu wa serikali na mwananchi ambapo ni pamoja na kushiriki katika miradi ya maendeleo hususan uchangiaji wa hiari na kuwasilisha maamuzi hayo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ili kupata kibali, wasilazimishwe,” alisema Mhe. Silinde.

Naye Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akichangia hoja katika suala hio ametoa wito kwa wazazi kuona umuhimu wa kushirikiana na serikali kujenga mazingira mazuri ya upatikanaji wa elimu iliyo bora.

"Nitoe wito kwa wazazi kuendelea kuona umuhimu wa kushirikiana na serikali kwa sababu mazingira yanapokuwa mazuri watoto wanakuwa na uhakika wakupata elimu iliyo bora, tunachosisitiza ni marufuku mwanafunzi afukuzwe shule sababu ya michango,” amesema Waziri Prof. Ndalichako.