Thursday , 19th May , 2022

Uongozi wa Klabu ya Simba umekiri kuwa nafasi yao kuutetea Ubingwa wa Ligi Kuu imekuwa finyu kutokana na matokeo ambayo wameyapata jana baada ya sare ya bao moja dhidi ya waoka mikate wa Azam Fc.

Ahmed Ally-Afisa Habari wa Simba

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa matokeo ya jana yameendelea kuwapa faida wapinzani wao Yanga ambao wanaongoza Ligi kwa tofauti ya alama 10 dhidi yao huku wakiwa wamesalia na mechi sita kuumaliza msimu huu.

''Tumeendelea kuwapa faida wapinzani wetu,asilimia kubwa kwa sasa zimeelekea kwao,lakini tunaendelea kupigana ingawa mambo yamezidi kuwa magumu, na kila mwana Simba anapaswa kuelewa hilo kuwa mambo ni magumu''Ahmed Ally.

Simba ilisawazisha bao kupitia John Bocco kufuatia Azam kutangulia kwa bao la Rodgers Kola ambalo liliwaamsha wana Msimbazi kujitutumua na kulazimisha sare hiyo.

Matokeo hayo yameipunguzia mzigo Yanga ambayo sasa itahitaji ushindi kwenye mechi tatu kati ya sita zilizosalia ili ifikishe alama 69 ambazo hata kama mabingwa watetezi wakishinda mechi zote zilizosalia watafikisha alama 68 ambazo hazitotosha kuwafanya watetee ubingwa.