Sunday , 4th Sep , 2022

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhishwa na namna serikali ilivyowajali wananchi waliohamia Kijiji cha Msomera kwa hiari yao wenyewe ili kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Ally Makoa

Akizungumza baada ya kutembelea Kijiji cha Msomera, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Ally Makoa, licha ya kutoa pongezi hizo amesema kamati yake imeshuhudia mambo makubwa yaliyotekelezwa na serikali ndani ya muda mfupi ili kuwafanya wakazi waliohamia kwa hiari katika kijiji hicho wawe na maisha bora zaidi.

"Leo tumejionea wenyewe majengo bora kabisa ya madarasa na vifaa vya kisasa vya kufundishia na mazingira yake, nyumba nzuri, maji ya kutosha, majosho mazuri ya wanyama, barabara inayopitika vizuri, hakika Wizara ya Maliasili na serikali kwa ujumla mnahitaji pongezi sana," amesema

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana, amemshukuru Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, kwa kuridhia kamati hiyo iende Kijiji cha Msomera kuona kazi nzuri inayoendelea kufanywa na serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Waziri Balozi Dkt. Chana, ameongeza kuwa Wizara anayoiongoza itaendelea kushirikiana kikamilifu na Wizara zingine katika kuhakikisha mazingira ya Kijiji cha Msomera kinazidi kuwa rafiki kwa wakazi wake na kwa wote wanaoendelea kuhamia kwa hiyari yao.