Thursday , 8th Sep , 2022

Serikali imetangaza kulegeza masharti ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19, ambapo kuanzia sasa hakutakuwa na ulazima wa kuvaa barakoa isipokuwa kwa mtu mwenye mafua pale itakapomlazimu sambamba na kwenye misongamano ya watu.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kufuatia kupungua kwa maambukizi ya ugonjwa huo hapa nchini na duniani na kwamba serikali pia imesitisha matumizi ya vipima joto kwa wasafiri baada ya kuona kwamba havisaidii.

Akitoa takwimu za vifo na maambukizi ya ugonjwa huo, Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya Dkt. Beatrice Mutayoba, amesema vifo na maambukizi tangu kuingia kwa ugonjwa huo nchini vimeshuka kwa asilimia kubwa kutokana na chanjo waliyoipata Watanzania na kufikia asilimia 60 ya Watanzania wote waliochanja

Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo Profesa Abel Makubi, amesema serikali imeongeza umri wa watoto wanaoingia nchini toka nje ya nchi ambao watalazimika kupimwa ugonjwa huo ni wale wenye umri wa kuanzia miaka 12 badala ya miaka mitano ilivyokuwa awali

Ugonjwa wa UVIKO-19 mpaka sasa umeua watu 808 nchini Tanzania huku wagonjwa waliothibitishwa mpaka sasa wakiwa ni 35,747.