Friday , 18th Nov , 2022

Serikali ya Tanzania imekemea urasimu wa upatikanaji wa Tin namba kwa wafanyabiashara na kuacha kutoa vitisho kwa wafanyabiashara wakati wa ukusanyaji wa kodi.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye akikabidhi tuzo kwa mshindi wa jumla wa tuzo za mlipa kodi bora 2021/2022

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Moses Nnauye wakati wa utoaji wa tuzo kwa walipa kodi bora 2021/2022 huku akiwataka TRA kufanya kazi kwa ukaribu na walipa kodi kwani wao ndio wadau wao wa muhimu.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango , Hamad Hassan Chande amesisitiza walipa kodi kutatuliwa changamoto zao ikiwa pamoja na Makadirio ya kodi yasiyoendana na mapato na kufungwa kwa biashara kwa wasio na Mashine za EFD.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Alphayo Kidata ameishukuru serikali kwa namna inavyolipa kipaumbele suala la usimamizi wa ulipaji wa kodi ambapo TRA imekuwa ikiongeza ufanisi wa makusanyo ya kodi huku akiahidi kuongeza matumizi ya TEHAMA katika ukusanyaji wa kodi.

Kwa upande wao washindi wa tuzo wamebainisha kuwa tuzo hizo zitachochea ulipaji kodi kwa hiari, jambo litakalosaidia ukuaji wa uchumi wa taifa na kuliletea maendeleo taifa.