Jumamosi , 14th Nov , 2020

Jeshi la Polisi mkoa wa Ruvuma, linamshikilia Christopher Njako (20), maarufu kama Bilionea wa Mkako kwa kosa la kutakatisha fedha baada ya kufanya biashara ya mahindi, akinunua mahindi hayo kwa zaidi ya Tsh. 70,000 kwa kila gunia na kisha kuuza kwa Tsh. 42,000 kwa kila gunia.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, ACP Simon Marwa Maigwa.

Akizungumza na EATV Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, ACP Simon Marwa Maigwa, amesema kuwa baada ya wananchi kuona kijana huyo akinunua mahindi kwa bei nzuri walianza kumuamini na kukimbilia kwake kuuza mahindi, huku wengine wakimkopesha lakini alishindwa kuwalipa hela zao na ndipo malalamiko yalipoanza.

"Biashara imekwenda ilipofika mwanzoni mwa mwezi wa 10, yakajitokeza malalamiko kwamba kuna watu wanamdai, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa ikamsimamisha kununua mahindi ili alipe kwanza madeni ya wakulima na wafanyabiashara wa mahindi lakini alikuwa anatoa ahadi zisizotetelezeka", amesema ACP Maigwa.

Aidha Kamanda Maigwa ameongeza kuwa, " Alijaribu kutoroka kitendo ambacho kiliashiria kabisa ni nia mbaya, watu wanaomdai ni zaidi ya 1200 na pesa anazodaiwa kuwa ni zaidi ya Bilioni 1.3, kitendo hicho kilileta mashaka baada ya hapo alikamatwa kwa makosa ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, utakatishaji wa fedha na atafikishwa mahakamani".