Ijumaa , 18th Jul , 2014

Kamati kuu ya Chama cha Mapinduzi nchini Tanzania CCM imewatahadharisha wanachama wake walioonesha nia ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kuwa wanaweza wakapoteza sifa za kugombea nafasi hiyo.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama tawala nchini Tanzania CCM, Nape Nnauye.

Wanachama na makada hao wanaweza kupoteza sifa hiyo iwapo hawatazingatia katiba, Kanuni na taratibu za chama zinazosimamia masuala hayo.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari jijini Dar es salaam juu ya maadhimio ya kamati kuu ya chama hicho iliyokutana chini ya mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye amesema kumekuwa na baadhi ya wanachama wa CCM ambao wanatangaza nia ya kugombea urais kupitia chama hicho bila ya kufuata taratibu.

Aidha Nape amesema wale ambao wameshapewa adhabu na kamati kuu kutokana na kukiuka baadhi ya taratibu za chama kwa suala hilo, kamati kuu ya usalama na maadili ya CCM itafanya mapitio ya mwenendo wao ya utekezaji wa adhabu hiyo na kama watabainika hawatekelezi ipasavyo wataongezewa adhabu.

Makada ambao mwenendo wao utaangaliwa ni pamoja Bernard Membe, Edward Lowassa, Frederick Sumaye, William Ngeleja na Stephen Wassira ambao wanaotwa kuwa katika kinyang'anyiro cha kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa Mwakani.

Kwa mujibu wa Nape, makada hao wa CCM walipewa miezi kumi na mbili ya uangalizi, muda ambao wanasiasa hao walitakiwa waonyeshe nidhamu kwa kufuata taratibu, sheria na miongozo ya chama ikiwa ni pamoja na kutofanya kampeni za mapema za kuwania urais.