Jumamosi , 14th Jan , 2023

Waziri wa Maliasili na Utalii Tanzania Balozi Dkt. Pindi Chana amesema hakuna ndege yoyote iliyotoka na mnyama katika hifadhi za Tanzania kama ilivyozushwa katika mitandao ya kijamii hivi karibuni 

Kauli hiyo ameitoa katika mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao (Zoom) ukiwakutanisha wadau mbalimbali wa uhifadhi na utalii nchini ambapo amesema serikali wanyama hao wanalindwa na sheria mbalimbali ikiwemo mikataba ya kimataifa hivyo sio rahisi kutokea tukio kama hilo

"Tunazo sheria ambazo zinalinda aina yoyote ya ujangili wa wanyama wetu, haitawezekana mtu yoyote, kutoa mnyama yoyote nchini bila kibali maalumu, wanyama hawa wanalindwa na sisi tupo katika mikataba ya kimataifa tumekubaliana wanyama tutaendelea kuwalinda"  

"Nichukue nafasi hii kuutangazia umma kuwa hakuna ndege iliyotoka na mnyama yoyote, wanyama hawa wanalindwa kwa mujibu wa sheria, lakini pia tunawalinda chini ya mikataba ya kimataifa, ndugu watanzania wanyama wetu wapo salama"

"Taarifa kwamba kuna ndege imekuja kuchukua wanyama hakuna, usafiri huo unakuja unaleta watalii na ndio maana tumeweka viwanja, sasa tumeweka viwanja alafu tusivitumie, si lazima tufike, mtu anafika anamaliza anawahi mkutano wake" amesema Balozi Dkt, Pindi Chana

Aidha Waziri Chana amesema kuwa watalii mbalimbali wamekuwa wakiingia katika hifadhi zetu kutokana na kuboreshwa kwa miundombinu mbalimbali

"Tulipitisha pale bungeni tuboreshe viwanja vya ndege maeneo yafikike, viwanja vinavyokaribiana na hifadhi, sasa leo mgeni akija kwa ndege tena unasema ndege hiyo moja Dubai, kwa kweli ndugu zangu watanzania naomba tuwe wazalendo"

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa KADCO - Uwanda wa ndege wa KIA, Christine Mwakatobe amesema kutokana na jitihada za serikali kutangaza utalii sasa idadi imeanza kuongezeka na ndio maana ndege nyngi zinatua katika viwanja vyetu huku akishangaa wanaosema kuna ndege zinabeba wanyama kupeleka nje 

"Wananchi waelewe kuwa ndege ile sio mara ya kwanza kutua kwenye uwanja wa KIA, ilishatua huko nyuma, nilivyoona ile taarifa mitandaoni nilishanga sana kwa sababu hawa wanaokuja na ndege ni watalii"

"Huko nyuma tulilia sana wakati wa COVID - 19 kwamba hatuna biashara, watalii hawaji, sasa  serikali ya awamu ya sita imetoka imetangaza na kujenga mahusiano bora huko duniani, sasa tunaanza kupokea wageni wa hadhi tofauti tofauti, badala watu watafakari hilo wanaenda kubini stori ambazo hazima matiki"