Kabudi akanusha taarifa ya Azory Gwanda kufariki

Alhamisi , 11th Jul , 2019

Waziri wa Mambo ya Nje Palamagamba Kabudi, amesema hajathibitisha kuwa aliyekuwa mwandishi wa habari za uchunguzi wa gazeti la Mwananchi Azory Gwanda, kuwa amefariki Dunia na kueleza mpaka sasa vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kuanya uchunguzi.

Waziri Kabudi ametoa kauli hiyo akiwa Uingereza kwenye mkutano wa nchi za Jumuiya ya Madola ambao unalenga kujadili ya hali ya utawala bora, katia nchi hizo.

Akizungumza nchini Uingereza Kabudi amesema kuwa "mpaka sasa hakuna uthibitisho kuwa Azory yuko hai au amefariki, vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kuchunguza tukio hilo na matukio mengine, yaliyotokea katika machafuko ya Kibiti."

Aidha amesema kuwa "kuhusu kile nilichokisema, katika mahojiano yangu BBC , nilieleza kuwa tukio lililotokea Kibiti lilikuwa la kuhuzunisha, na wapo Watanzania waliouawa na wengine kupotea, sikuthibitisha kuwa Azory Gwanda amefariki."

Mapema Julai 11, 2019, wakati akifanya mahojiano maalum kuhusiana ahali ya usalama Tanzania kwenye kituo cha habari cha BBC Waziri Kabudi alisema kuwa "tatizo la Rufiji ni moja ya matukio yaliyoumiza na kusikitisha ambayo TZ tumeyapitia, pale Rufiji sio Azory Gwanda pekee ambaye amepotea na kufariki,nikuhakikishie tunachukua kila hatua, ili watu wetu wawe salama awe Mwanahabari,Polisi au raia wa kawaida."