Ijumaa , 13th Jan , 2023

Mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Mwanza imeonya upande wa Jamhuri kuhusu danadana za upelelezi kukamilka kwenye kesi namba 11 ya usafirishaji haramu wa binadamu inayomkabili Diana Bundala maarufu kama mfalme Zumaridi huku ikisema tarehe iliyopangwa ambayo ni tarehe 27 iwe ya mwisho

Kesi hiyo iliyoanza kutajwa tangu mwezi February mwaka jana lakini hadi leo upande wa jamhuri umekuwa ukisema upelelezi wake haujakamilika hali iliyosababisha wakili anayemtetea Zumaridi Erick Mutta kuiomba mahakama hiyo ikae na mawakili wa jamhuri ili waeleze nini kinakwamisha upelelezi huo licha ya mara ya mwisho kudai jalada la kesi hiyo limeshafikishwa mikononi mwa mkurugenzi mkuu wa mashtaka nchini DPP

Baada ya ombi hilo la wakili wa Zumaridi hakimu aliyesimamia kesi hiyo kwa siku ya leo Amani Sumari akaonya upande wa jamhuri kuhakikisha kesi hiyo itakapotajwa tena tarehe 27 ya mwezi huu wahakikishe upelelezi wa kesi hiyo unakamilika na kuacha kupiga danadana nan je ya mahakama wakili anayemtetea mfalme Zumaridi akaeleza

‘Na sisi kama mawakili upande wa utetezi tuliikumbusha mahakama wajibu wake wa kuona haki inatendeka tunaishukuru mahakama leo imetoa onyo kwa ofisi ya mwendesha mashtaka na kuitaka tarehe inayokuja terehe 27 wawe wamefanya maamuzi ya msingi ambapo tunatarajia maamuzi ya msingi katika jalada hilo twende kwenye hatua inayofuata’

Katika kesi nyingine namba 10 ya mwaka 2022 inayomkabili Diana Bundala maarufu kama mfalme Zumaridi na wafuasi wake nane ya kuwazuia maafisa wa serikali kutekeleza majuku yao ambayo leo hii ingetolewa hukumu imekwama baada ya hakimu Monica Ndyekobora anayesikiliza kesi hiyo kufiwa hali iliyomlazimu hakimu Amani Sumari kuiahirisha hadi tarehe 25 ya mwezi huu.