Jumanne , 14th Jul , 2020

Madaktari 44 katika Hospitali ya kujifungulia kina mama, iliyopo Pumwani jijini Nairobi, wamekutwa na Corona na kupelekea mgomo baridi wa wahudumu wa afya, huku Serikali ikisema imeweka mikakati kuwakinga wahudumu hao.

Mkurugenzi Mkuu kutoka Wizara ya Afya Kenya, Dkt Patrik Amoth,

Madaktari hao wamebainika hii ni baada ya wafanyakazi 290 kupimwa hospitalini hapo, na kufikisha idadi ya wahudumu wa afya 429 ambao wamekwishaambukizwa Virusi vya Corona, ikiwa ni sawa na asilimia 4.1 ya maambukizi yote nchini Kenya.

Mkurugenzi Mkuu kutoka Wizara ya Afya Kenya, Dkt Patrik Amoth, alipotembelea Hospitali hiyo hii leo Julai 14, 2020, baada ya kuripotiwa kuwepo mgomo baridi hospitalini hapo, amethibitisha idadi hiyo ya maambukizi, na kusema kuwa wote waliokutwa na Corona wanaendelea vizuri.

"Kati ya watu 290 waliopimwa, 44 wamepatikana na Corona, bado tuna watu 100 ambao hatujawapima, lakini napenda niseme kuwa wote hao 44 wanaendelea vizuri, wako katika hali nzuri , na wengi hawajaonyesha dalili hivyo wanajitenga nyumbani kwao" amesema Dkt Amoth.

Licha ya hayo Serikali ya Kenya imesema kuwa haitaifunga Hospitali hiyo, kwa kuwa inategemewa na kina mama wengi nchini humo hasa wa Kaunti ya Nairobi, na kusisitiza tahadhari kuchukuliwa, ikiwemo ujenzi wa chumba maalum cha madaktari kutengwa na kupimwa ambao umekamilika.