Alhamisi , 2nd Jul , 2020

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda amekabidhi mradi wa hospitali ya Kivule kwa Chama cha Mapinduzi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa miradi mbalimbali kupitia ilani ya chama hicho.

Paul Makonda akiwa anaongea na waandishi pamoja na wananchi wa kivule leo Julai 2, 2020.

Akizungumza katika ziara yake katika Jimbo la Ukonga Makonda amesema, Hospitali hiyo ina majengo 7 na mpaka sasa imeshahudumia zaidi ya watu 1000 na inatoa huduma za X-ray, OPD na nyinginezo.

Sehemu ya majengo na eneo la hospitali ya Kivule

Aidha katika huduma za mama na mtoto tayari zaidi ya kinamama wajawazito 30 wamepatiwa huduma za kujifungua katika hospitali hiyo.

Hata hivyo Makonda amezungumza na wananchi, katika soko la Kivule na kusema serikali inaendelea na ujenzi wa barabara zitakazorahisisha usafirishaji wa bidhaa zao ili kuondoa adha ya usafiri.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dar es salaam Kate Kamba, amesema utekelezwaji wa miradi mbalimbali katika Jimbo la Ukonga ni hatua mojawapo za utekelezaji wa ilani ya CCM chini ya Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli.