Jumanne , 31st Jan , 2023

Rais wa Marekani Joe Biden amefutilia mbali uwezekano wa kutuma ndege za kivita za F-16 nchini Ukraine, licha ya wito mpya kutoka kwa maafisa wa Ukraine wa kuomba msaada wa ulinzi wa anga.

Rais wa Marekani Joe Biden

Kauli yake inakuja siku moja baada ya kiongozi wa Ujerumani pia kukataa kutuma ndege za kivita ambapo Ukraine imesema inahitaji ndege hizo kuchukua udhibiti wa anga yake katika vita vinavyoendelea dhidi ya Urusi.

F-16 Fighting Falcons inachukuliwa sana kuwa mojawapo ya ndege za kivita zinazotegemewa zaidi duniani na hutumiwa na nchi nyingine, kama vile Ubelgiji na Pakistan.

Hata hivyo, Bw Biden amepinga mara kwa mara ombi la Ukraine la kutaka ndege hizo, badala yake akalenga kutoa msaada wa kijeshi katika maeneo mengine huku Marekani ikitangaza kuipatia Kyiv vifaru 31 vya Abrams, huku Uingereza na Ujerumani pia zikiahidi msaada sawia na huo.