Jumanne , 18th Jun , 2019

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amependekeza kuongezwa kwa wigo wa walipa kodi, ili kuwaondolea mzigo baadhi ya watumishi na wafanyakazi kazi sekta mbalimbali nchini.

Nape ametoa kauli hiyo kwenye mjadala wa Bajeti bungeni jijini Dodoma wakati akizungumzia juu ya mgawanyo wa fedha hususani kwenye sekta ya Kilimo, ambayo imeonekana ikiongoza kwenye uchangiaji wa pato la taifa.

"Wigo wa walipa kodi kwa muda sasa kuna takwimu kwamba walipa kodi milioni 14 wanaolipa milioni 2.4, mzigo wa walipa kodi wengi unabebwa na walipa kodi wachache, nadhani huu wigo tungeanza nao kidogo kidogo ili tuweze kupunguza kodi kwa wafanyakazi", amesema Nape.

"Wapo walimu ambao wengi wanateseka, tunategemea PAYE kama biilioni 194, lakini tungeikata kwa nusu ingekuwa bilioni 97 huu mzigo tungeitafuta sehemu nyingine kwa walipa kodi ambao tutakuwa tumeongeza wigo", amesema Nape.

Kwa sasa Bunge linaendelea jijini Dodoma ambapo Wabunge wanajadili suala Bajeti ya 2019/2020 ambayo iliwasilishwa na Waziri wa Fedha Alhamisi ya wiki iliyopita.