Jumatatu , 21st Oct , 2019

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya albert Chalamila, amesema na yeye alishawahi kucharazwa bakora hadharani, wakati akiwa anasoma elimu ya Sekondari na kudai kuwa bakora hizo ndiyo zilizomsaidia mpaka sasa amekuwa Mkuu wa Mkoa, pamoja na kushika nafasi zingine za uongozi kwenye siasa.

Chalamila ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na EATV / EA Radio Digital, kuhusiana na hatma ya wanafunzi wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari Kiwanja, ambao aliwatimua kurudi nyumbani na kuwataka kulipa faini ya shilingi laki 2 kila mmoja, ambapo amesema mpaka sasa jumla ya wanafunzi 207 wameshalipa.
 

Mimi ni Mwalimu nimeshafundisha Shule za Sekondari 17, na Vyuo Vikuu kwa hiyo mimi ninatandika sana, nimeshawahi kuwa Mkuu wa Shule na baada ya hapo ndiyo nikaacha nikahamia kwenye masuala ya siasa."amesema Chalamila.

Aidha Chalamila ameongeza kuwa, "Kuhusu mimi kuchapwa hadharani nimeshachapwa sana wakati nikiwa nasoma tena nipiga karibia mara saba na nimechapwa kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo makosa ya kutofanya usafi, kuleta migomo na kusababisha migomo, na hata siku ya mwisho ya mtihani wangu wa form four nilipotoka kwenye mtihani wangu wa hesabu nilichapwa na Mwalimu wangu Robert".

Leo Jumatatu Mkuu huyo wa Mkoa, anatarajiwa kutoa hatma ya wanafunzi 56 wa Shule ya Sekondari Kiwanja , ambao aliwatimua Shuleni na kuwataka kulipa faini kwa tuhuma za kutishia kuchoma moto mabweni.